Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, mfululizo wa tafiti za Mahdawiyya zikiwa na anuani isemayo “Kuielekea Jamii Bora” kwa lengo la kueneza mafundisho na elimu kumhusu Imam wa Zama, Imam Mahdi (aj), na zinawasilishwa kwenu nyinyi wasomi wapendwa.
(Baadhi ya Aya zinazohusiana na Imam Mahdi (aj) na Mapinduzi Yake kwenye Ulimwengu ni kama zifuatazo:)
Aya ya Tatu
«وَعَدَ اللَّهُ الَّذینَ آمَنُوا مِنْکُمْ وَ عَمِلُوا الصَّالِحاتِ لَیسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِی الْأَرْض کَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذینَ مِنْ قَبْلِهِمْ وَ لَیمَکِّنَنَّ لَهُمْ دینَهُمُ الَّذِی ارْتَضی لَهُمْ وَ لَیبَدِّلَنَّهُمْ مِنْ بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْناً یعْبُدُونَنی لا یشْرِکُونَ بی شَیئاً وَ مَنْ کَفَرَ بَعْدَ ذلِکَ فَأُولئِکَ هُمُ الْفاسِقُونَ.»
Mwenyezi Mungu amewaahidi wale miongoni mwenu walioamini (walio muamini Mungu na Hujjat wa zama, (as) na wakatenda mema kwamba (katika zama za kudhihiri kwa Imam Mahdi) atawafanya warithi katika ardhi, kama alivyowafanya warithi wale waliokuwa kabla yao; na atawaimarishia dini yao aliyowachagulia (ambayo ni Uislamu wa kweli juu ya dini zote). Na baada ya hofu na woga wao, atawabadilishia usalama kamili, ili wanabudu Mimi peke Yangu bila kushirikisha chochote. Na atakayekufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu wa kweli.
(Surat An-Nur, Aya ya 55)
Katika aya zilizo kabla ya hii, kumezungumziwa utiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (saww). Aya hii inaendeleza maelezo hayo kwa kubainisha matokeo ya utiifu huo — yaani kuutawala ulimwengu mzima.
Aya hii inaonyesha kuwa Mwenyezi Mungu amewapa waislamu wema na waumini vitu vitatu:
1. Urithi na utawala juu ya ardhi;
2. Kuieneza haki ulimwenguni;
3. Kuondolewa kwa hofu na ukosefu wa usalama.
Matokeo yake ni kwamba; watu katika zama hizo watamwabudu Mwenyezi Mungu kwa uhuru kamili, watamtii kwa moyo wote, hawatamahirikisha na yeyote, na wataieneza tauhidi safi kila sehemu duniani.
Nukta Muhimu
1. Kwa mujibu wa aya hii, kabla ya Waislamu pia walikuwepo watu waliowahi kupewa ukhalifa juu ya ardhi. Wao ni wakina nani?
Baadhi ya wafasiri wamelifasiri hili kama linamhusu Nabii Adam, Nabii Daud, na Nabii Sulayman (as), kwa sababu Qur’ani inasema kumhusu Nabii Adam (as):
«إِنِّی جاعِلٌ فِی الْأَرْضِ خَلِیفَة.»
Mimi nitamweka khalifa (mwakilishi) katika ardhi.
(Surat Al-Baqarah, Aya 30)
Na kuhusiana na Nabii Daud (as) inasema:
«یا داوُدُ إِنَّا جَعَلْناکَ خَلِیفَةً فِی الْأَرْض.»
Ewe Daud! Hakika tumekufanya uwe khalifa (mwakilishi Wetu) katika ardhi.
(Surat Swad, Aya 26)
Nabii Sulayman (as) vile vile, kwa mujibu wa Aya ya 16 ya Surat An-Naml, alirithi ufalme wa Nabii Daud (as) na akawa khalifa katika ardhi.
Hata hivyo, baadhi ya wafasiri kama Allāmah Ṭabāṭabā’ī (ra) wameiona tafsiri hii ipo mbali, kwani tamko «الَّذینَ مِنْ قَبْلِهِمْ» halitumiki kwa manabii katika Qur’ani. Kwa mtazamo wake, aya hii inahusiana na umma zilizotangulia ambazo zilikuwa na imani na matendo mema, hivyo zikapewa utawala duniani.
Wengine wameiona aya hii inawahusu Bani Isra’il, kwa sababu alipo dhihiri Nabii Musa (as) na utawala wa Firauni ulipovunjwa, walipewa utawala juu ya ardhi. Kama Qur’ani inavyosema:
«وَأَوْرَثْنَا الْقَوْمَ الَّذینَ کانُوا یسْتَضْعَفُونَ مَشارِقَ الْأَرْضِ وَمَغارِبَهَا الَّتی بارَکْنا فیها.»
Na tukawarithisha watu walio kuwa wanadharauliwa mashariki na magharibi ya ardhi tuliyo ibariki.
(Surat Al-A‘rāf, Aya 137)
Na tena Qur’ani inasema kuwahusu wao:
«وَ نُمَکِّنَ لَهُمْ فِی الْأَرْض.»Tumenuia kuwapa nguvu na mamlaka katika ardhi (yaani waumini wa Bani Isra’il).
2. Ahadi hii ya Mwenyezi Mungu ni kwa nani?
Katika aya hii, Mwenyezi Mungu amewaahidi waumini na watu wema, utawala kwatika ardhi, utukufu wa dini, na usalama kamili. Lakini ni kundi gani hasa? Kuna mjada katika hili kwa wafasiri.
Baadhi ya wafasiri wameona kwamba aya hii inahusu Imam Mahdi (aj), ambaye katika zama zake mashariki na magharibi ya dunia zitakuwa chini ya bendera yake tukufu. Dini ya haki itaenea kila mahali, hofu na vita vitaondoka, na ibada safi pasi na kumshirikisha Mola itatekelezwa ulimwenguni kote.
(Tafsiri al-Mīzān, Juzuu ya 15, uk. 218)
Bila shaka yoyote, aya hii inawahusu Waislamu wa mwanzo pamoja na dola ya Imam Mahdi (aj). Kwa mujibu wa itikadi ya Waislamu wote — wawe ni Shia au Sunni — Imam huyo mtukufu ataujaza ulimwengu uadilifu na haki, na yeye ndiye mfano kamili wa maana ya aya hii. Hata hivyo, jambo hili halizuii uwepo wa ujumla na upana wa dhana ya aya hiyo.
Hili la kuwa baadhi wanasema kuwa neno «أرض» (ardhi) ni neno lililoachwa wazi na linamaanisha dunia nzima, na hivyo aya hii inamhusu peke yake Imam Mahdi (aj), hawako sahihi kabisa; kwa sababu kauli «کما استخلف...» (kama alivyo wafanya waliokuwa kabla yao kuwa makhalifa) haiendani na hilo. Hii ni kwa sababu ukhalifa wa waliokuwa kabla haukuwa utawala wa dunia nzima, bali sehemu maalum tu.
Ukiachilia mbali hilo, sababu ya kushuka kwa aya hii inaonesha kwamba, kwa uchachr mfano wa awali, aina ya utawala huu ulipatikana katika zama za Mtume (saww), ingawa ulikuwa ni katika kipindi cha mwisho cha uhai wake mtukufu.
Ni vyema kufahamu kwamba matunda ya jitihada za Mitume wote, juhudi zao za kudumu katika wito wa tauhidi, pamoja na mfano kamili wa utawala wa umoja wa Mwenyezi Mungu, amani kamili, na ibada safi, yatadhihirika kwa ukamilifu wakati Imam Mahdi (ajtf) atakapo dhihiri.
(Tafsiri ya al-Namūneh, juzuu ya 14, uk. 530–532)
Kama ilivyotajwa hapo awali, tafsiri hizi hazimaanishi kuwa aya hii imebinafsishwa kwake pekee, bali zinabainisha kuwa yeye ndiye mfano kamili zaidi wa maana yake.
Abu Basir amepokea kutoka kwa Imam Ja‘far al-Sadiq (as) kwamba Mtume huyo alisema kuihusu aya hii:
«نَزَلَتْ فِی اَلْمَهْدِیِّ عَلَیْهِ اَلسَّلاَمُ.»
Yaani, [aya hii] imeteremshwa kuhusiana na al-Qa’im (Imam Mahdi (aj) na wafuasi wake.
(Shaykh al-Tusi, Kitāb al-Ghaybah, uk. 177)
Allāmah Ṭabāṭabā’ī (ra) anaandika kuhusu jambo hili akisema:
“… Jamii safi na takatifu yenye sifa hizi za utukufu na usafi haijawahi kuundwa duniani tangia Mwenyezi Mungu alipomtuma Mtume (saww) hadi leo. Kwa hiyo, jamii kama hiyo haitapatikana ila katika zama za Imam Mahdi (ajtf), kwa kuwa hadithi nyingi mutawatir kutoka kwa Mtume (saww) na Maimamu wa Ahlul-Bayt (as) zimeeleza juu ya sifa za zama hizo na jamii hiyo.”
Kisha anaongeza:
“Huenda mtu akauliza: Ikiwa hivyo ndivyo, kwa nini basi Qur’ani imewaelezea wasikilizaji wa wakati ule, ikisema ‘wale walioamini na wakatenda mema’, ilhali Imam Mahdi (aj) hakuwepo wakati huo, wala yeyote wa zama zake?
Jibu ni kwamba swali hilo linatokana na kuchanganya kati ya anuwani za mtu binafsi na zile za kijamii.
Kwa maana kwamba, kauli ya Qur’ani inaweza kuelekezwa kwa watu kwa njia mbili:
1. Kwa maana ya kuwahusu wao kama watu binafsi;
2. Au kuwahusu wao kama jamii yenye sifa fulani maalum.
Katika namna ya kwanza, kauli hiyo inahusu watu hao pekee — ahadi na onyo havihusiani na wengine.
Lakini katika namna ya pili, watu hao hawana nafasi binafsi; bali kauli inawahusu watu wote wenye sifa hizo popote na wakati wowote.
Katika aya hii, kauli ni ya namna ya pili. Ndivyo ilivyo kwa aya nyingi za Qur’ani zinazowahutubia waumini au makafiri.”
(Tafsiri al-Mīzān, juzuu ya 15, uk. 220, tafsiri ya Kiswahili)
Katika Majma‘ al-Bayān, chini ya aya
«وَعَدَ اللَّهُ الَّذینَ آمَنُوا مِنْکُمْ...»imeandikwa kwamba wafasiri wamekhitalifiana juu ya maana ya
«الذینَ آمَنُوا مِنکُم»ni akina nani hawa?
Imepokelewa kutoka kwa Ahlul-Bayt (as) kwamba kinachokusudiwa ni Mahdi kutoka katika kizazi cha Muhammad (saww).
Al-‘Ayyāshī amepokea kwa sanad yake kutoka kwa Ali ibn al-Husayn (as) kwamba alipokuwa akisoma aya hii, alisema:
“Naapa kwa Mwenyezi Mungu! Hao ni Shia wetu, watu wa nyumba ya Mtume, ambao Mwenyezi Mungu atatekeleza ahadi hii kupitia mtu mmoja miongoni mwetu — naye ni Mahdi wa umma huu.
Yeye ndiye ambaye Mtume (saww) amesema kuhusiana naye:
‘Lau kama dunia ingelibakia siku moja tu, basi Mwenyezi Mungu angeirefusha siku hiyo hadi atakaposimama mtu mmoja kutoka katika kizazi changu, ambaye jina lake ni jina langu. Yeye ataijaza ardhi haki na uadilifu kama ilivyokuwa imejaa dhulma na uonevu.’”
Hadithi yenye maana sawa na hii imepokelewa pia kutoka kwa Imam Muhammad al-Baqir (as) na Imam Ja‘far al-Sadiq (as).
Utafiti huu unaendelea..
Imenukuliwa kutoka katika kitabu kiitwacho “Darsnāmeh-ye Mahdawiyyat” kilichoandikwa na Khudā-Murād Salīmiyān, huku ikifanyiwa marekebisho kiasi.
Maoni yako